RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

BAA YAGEUZWA KANISA JIJINI DAR


WAKATI matukio mengi ya kushangaza na kushtukiza yakiendelea kutokea kila siku duniani, neno la Mungu nalo linazidi kushika kasi kufuatia baa moja iliyopo Sinza-Lion jijini Dar kugeuzwa kuwa kanisa.


Baa iliyopo Sinza-Lion jijini Dar ambayo imegeuzwa kuwa kanisa.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baa hiyo maarufu iitwayo The Don, ukumbi wake ambao ulikuwa ukitumika kwa watu kupiga ulabu, hivi sasa unatumiwa na waumini wa kanisa linalojukana kama Impact International Christian Centre kupata mahubiri.

Lakini cha kushangaza ilibainika kwamba katika maandishi makubwa yanayolinadi jina la baa hiyo, chini yake ndipo limewekwa bango linaloonyesha kanisa hilo, kitu ambacho kwa mtu mgeni, ni vigumu kuelewa mara moja.


Muonekano wa karibu wa kanisa hilo.


“Siyo baa hiyo kaka, hilo ni kanisa siku hizi, tumeshangaa ghafla tu waumini wanakuja na mhubiri wao na wanaendelea na sala kama kawaida. Hatujui kama huyu mhubiri ndiye alikuwa mmiliki wa hii baa au imekuwaje,” alisema jirani mmoja wa eneo hilo, aliyekataa kutaja jina.

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kuzungumza na uongozi wa baa au kanisa hilo ziligonga mwamba baada ya kuambiwa na majirani kuwa ni nadra kuwakuta mahali hapo hivyo jitihada zinaendelea. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kuibuka kwa makanisa ya madhehebu mbalimbali, ambayo kila moja huwa na watumishi wao wanaopewa majina kama Mchungaji, Nabii, Askofu na kadhalika.

Comments