RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

JE WAJUA! KAKOBE ALIWAHI KUWA MWANAMUZIKI

Mjue huyu ni safu mpya ambayo itakuwa inahusisha watu maarufu ambao watakuwa wakihojiwa na waandishi wetu wakielezea historia yao tangu wakiwa wadogo hadi kuwa maarufu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (F.G.B.F), Zachary Kakobe.

Tunaanza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (F.G.B.F), Zachary Kakobe ambaye amefanikiwa kuanzisha kanisa hilo ambalo limesambaa nchi nzima na nje ya nchi.
Ana historia ndefu na safu hii itakuwa inakuletea mfululizo wa historia yake kama anavyojieleza akiwa makao makuu ya kanisa hilo lililopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam.

Mwandishi: Kwanza kabisa waambie wasomaji wetu, umezaliwa lini na wapi?

Askofu Kakobe: Mimi ni Mtanzania, nimezaliwa Jumapili ya Juni 6, mwaka 1955, Kibondo, Kigoma Tanzania, nimesoma shule ya msingi huko na kidato cha sita nimemalizia Mkwawa, Iringa.
Mwandishi: Uliokoka lini na nani alikushawishi hadi ukaokoka?

Askofu Kakobe; Safari yangu ya wokovu ilianza Jumapili ya Sikukuu ya Pasaka Aprili 6, mwaka 1980 baada ya kuhudhuria mkutano wa Injili ambao ulikuwa ukihubiriwa na Askofu Moses Kulola katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Ilala, Dar es Salaam, chini ya uandalizi wa Mchungaji Titus Mukama.
Siku hiyo neno la wokovu lililohubiriwa na Askofu Kulola lilinifanya niende mbele yake huku nikilia hadharani na nikatubu dhambi zangu kutoka moyoni na nikijiapia kumfuata Yesu kuwa bwana na mwokozi wangu.

Askofu Zachary Kakobe akiwa na mkewe.

Kabla ya hapo nikiwa shule nilikuwa mpenda muziki na tulikuwa na bendi pale. Baada ya hapo niliendelea kufanya kazi mbalimbali lakini baadaye nikawa nina studio ya kurekodi, Temeke Dar.

Mwandishi: Baada ya kuokoka nini kilifuata?

Askofu Kakobe: Kutoka siku hiyo nilibadilika moja kwa moja na mke wangu pamoja na marafiki zangu walikuwa mashahidi kwamba nimebadilika na maisha yangu yalibadilika. Nilikuwa kiumbe kipya, nilizaliwa upya katika dunia hii.

Mwandishi: Baada ya kuokoka ulijiunga na kanisa gani?

Askofu Kakobe: Mara tu baada ya kuokoka nilijiunga na kanisa la Tanzania Assemblies of God, Temeke, Dar es Salaam na kwa miaka mingi nilikuwa katika kanisa hilo lililokuwa likiongozwa na marehemu Mchungaji Callist Masalu, ambaye alikuwa mtumishi wa Mungu nchini kwa zaidi ya miongo minne. Nilipata uzoefu mkubwa wa jinsi ya kumtumikia Mungu katika kanisa hilo.

KUTOKEWA NA YESU
Mwandishi: Nini kiliendelea baada ya hapo?

Askofu Kakobe: Nakumbuka mwaka 1982, nilitokewa na Bwana Yesu katika chumba changu cha kulala, mara mbili kwa nyakati na akanipa ujumbe wa kuanzisha huduma.

Bwana Yesu alikuwa akinitokea mapema usiku hata kabla familia haijalala, ipo living room (chumba cha maongezi). Mara ya kwanza alinigongea mlango ambao nilikuwa nimeufunga kwa funguo. Chakushangaza ni kwamba hata kabla sijafungua, akawa ameingia chumbani.

Mwandishi: Alipoingia Yesu chumbani kwako, mambo yalikuwaje au ulijisiakiaje?

Askofu Kakobe: Mara baada ya Bwana Yesu kuingia chumbani mwangu taa za umeme zilizimika ghafla bila mtu yeyoye kuzizima, nilipigwa na butwaa! Lakini utukufu wake ukajaa katika chumba,
aliketi kitini na kuniambia “Usihofu, mimi ni Yesu”, akasema ananituma kuhubiria neno lake! Akasema; Kakobe utakuwa ngao kwa kondoo wengi waliopotea na utahubiri wokovu kwa maelfu ya kondoo hao na wengine wengi watakaokukimbilia.

Wakati huohuo utahubiri utukufu wa Mungu ukianzia katika taifa lako na baada ya miaka utaeneza neno katika mataifa duniani. Aliniambia mambo mengi kuhusiana na Mungu na mipango yake kuhusu huduma nitakayotoa na alimalizia kwa kunisisitizia kuwa niwe mwaminifu kwake hadi mwisho wa maisha yangu.

Mwandishi: Ni mambo mazito. Ulipopewa kazi hiyo nzito, wewe ulimuambia nini?

Askofu Kakobe: Kusema kweli baada ya yeye kumaliza maelezo yake, hakunipa nafasi ya kujadiliana naye zaidi ya kunihakikishia kuwa atahakikisha atakuwa pamoja nami.
Aliondoka kwa kupitia palepale alipoingilia na kimaajabu kabisa taa za umeme zilizokuwa zimezimika, zikawaka ghafla tena bila kuwashwa na mtu yeyote.Mwandishi: Ulifanya nini baada ya kupewa jukumu hilo zito?Itaendelea wiki ijayo, usikose.

Comments