RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SAKATA LA GWAJIMA, MAASKOFU WAWASHANGAA POLISI

Na Elvan Stambuli
Maaskofu kadhaa wamelishangaa jeshi la polisi kwa jinsi lilivyoliendesha sakata la kashfa ya matusi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na kusema kwamba huenda kuna jambo nyuma ya pazia.


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.


Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya maaskofu hao walisema sakata hilo sasa limeingizwa kinyemela kwenye mlango mwingine usiojulikana badala ya madai ya awali kwamba Askofu Gwajima alimkashifu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kadinali Pengo.

Akizungumza kwa niaba ya maaskofu wa Kipentekoste ambao ni marafiki wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Dk. Rejoice Ndalima alisema hawaelewi polisi wana maana gani kubadili tuhuma za Askofu Gwajima za kumtukana Askofu Pengo na kutakiwa kupeleka vithibitisho vya mali anazomiliki na kuulizwa masuala ya ndugu zake walio hai na waliofariki dunia.

“Tumejiuliza sana sisi maaskofu kwamba jeshi la polisi linataka nini sasa kwa Askofu Gwajima. Hatuoni kama ni sawa kwao (polisi) kumhoji Gwajima umiliki wa mali zake kwenye kesi ya kumtukana Pengo, sioni kama hiyo ni kazi yao,” alisema Askofu Dk. Ndalima.

Akifafanua zaidi, askofu huyo alisema kwamba kazi ya kutaka vithibitisho vya umiliki wa mali au kama analipa kodi au la na kazipataje ni kazi ya mamlaka nyingine za serikali, hivyo polisi wanapaswa kufanya kazi yao ya ulinzi wa raia na mali zao.

Alisema kuhusu kiwanja cha Tanganyika Packers ambacho Askofu Gwajima na kanisa lake wanakitumia kufanyia ibada, hakuvamia bali aliruhusiwa na serikali, hivyo polisi wanataka kuleta mgongano wa kimamlaka.
Askofu Dk. Ndalima alisema kutokana na hayo waliyoyaona, sasa wanafanya utaratibu ili kuonana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu ili kujua uhalali wa askari wake kufanya wanachokifanya sasa.

“Tulishaonana na IGP Mangu wakati sakata hili linaanza na alitupa matumaini kuwa litamalizika mapema na kwa kutumia busara... sasa jeshi kuhama polepole katika ajenda ya msingi na kuibua nyingine kunatupa shaka,” alisema askofu huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu David Mwasota (pichani) amesema maaskofu wa baraza hilo wanashangaa kusikia polisi wanahitaji hati ya usajili wa kanisa la Gwajima na kuacha tuhuma walizomuitia.

“Tumeona tusijibu sasa labda serikali imeona kuna kitu kwa sababu ina mkono mrefu... wametuacha kwenye njia panda, baraza litazungumza baada ya Askofu Gwajima kupeleka hati,” alisema Askofu Mwasota. Tayari wakili wa Askofu Gwajima, John Mallya amesema alishawaandikia barua polisi kuwaambia vyote walivyotaka kwa Askofu Gwajima wawaandikie barua na isiwe kwa maneno kama walivyofanya awali.

Alipoulizwa kama haoni kuwa hiyo inaweza kuwa mbinu ili Gwajima afutiwe usajili wa kanisa lake, alisema polisi hawana uwezo wa kufanya hivyo au kumpora hati Gwajima bali kinachofanyika ni usumbufu usio na maana kwa sababu chombo cha serikali kinachosajili makanisa kipo Wizara ya Mambo ya Ndani, chini ya ghorofa za makao makuu ya jeshi hilo la polisi.

Askofu Gwajima anatakiwa na polisi kupeleka Makao Makuu ya Kanda Maalum ya Kipolisi Dar, nyaraka mbalimbali zikiwemo hati ya kanisa, helikopta, nyumba yake na kadhalika Aprili 16, mwaka huu.